11/09/2026
Mkutano huo wa 67 wa Jumuiya ya Kusini mwa Afrika ya Nishati ya Umeme — SAPP, umewakutanisha viongozi na wataalamu kutoka nchi wanachama kwa ajili ya kujadili masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya umeme.
Mkutano huo umehudhuriwa pia na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), Mhandisi Haji Haji, pamoja na viongozi na wafanyakazi wa Shirika hilo, kwa lengo la kufuatilia kwa karibu majadiliano na utekelezaji wa masuala yanayohusu sekta ya umeme katika ukanda huo.
Mkutano wa 67 ulifunguliwa tarehe 7 Septemba 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa ZECO, Mhandisi Haji Haji, ambapo wajumbe walifanya majadiliano kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano katika sekta ya umeme.
Mkutano huo umefikia kilele leo, tarehe 11 Septemba 2026, ambapo kikao cha viongozi wa Jumuiya hiyo kimefungwa na Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Zanzibar, Mheshimiwa Seif Kombo Pandu.
Mkutano huo wa SAPP umeandaliwa na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kwa kushirikiana na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO), ukiwa umejikita katika kuimarisha ushirikiano wa nchi wanachama katika sekta ya umeme, ikiwemo uzalishaji, usafirishaji na biashara ya nishati.
Ushirikiano huo unalenga kuhakikisha nchi wanachama zinakuwa na mifumo imara ya umeme, pamoja na uwezo wa kusaidiana pale zinapokabiliwa na changamoto za upatikanaji wa nishati.
Akizungumza wakati wa kufunga mkutano huo, Naibu Waziri wa Maji, Nishati na Madini Zanzibar, Mheshimiwa Seif Kombo Pandu, amesema Zanzibar ni miongoni mwa maeneo yanayoshiriki kikamilifu katika jitihada za kuimarisha sekta ya umeme, akieleza kuwa kupitia mkutano huo wanatarajia malengo yaliyowekwa yatafanikiwa.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Usafirishaji wa Umeme kutoka TANESCO, Mhandisi Zakaria Mgarama, amesema mkutano huo umeweka msisitizo katika ushirikiano wa nchi mbalimbali katika sekta ya umeme, jambo litakalosaidia kuongeza usalama wa nishati na kuwezesha nchi wanachama kusaidiana pale zinapokabiliwa na changamoto za umeme.
# #