16/12/2025
DAS SICHALWE AWATAKA WATENDAJI WA KATA NA VIJIJI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA MBARALI KUBEBA SURA YA SERIKALI KWENYE UTENDAJI KAZI
Katibu Tawala wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Ndugu Frank Sichalwe amewataka watendaji wa Kata na vijiji pamoja na Watumishi wote katika ngazi za vijiji na Kata kuhakikisha wanafanya kazi vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri.
Akizungumza katika kikao kazi kilichowakutanisha Watendaji Kata wote wa Kata za Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Ndugu Sichalwe amesema watendaji wote wa serikali ni picha halisi ya Serikali kwani utendaji wa kila Mtumishi, utoaji wa huduma ndio unabeba muonekano wa Serikali pamoja na Mheshimiwa Raisi,
"Sisi ni picha ya Serikali, ni picha ya Mheshimiwa Rais, ni picha ya Chama cha Mapinduzi, tusiitukanishe Serikali. Sura ya Serikali ni wewe unavyotoa huduma" Amesema Katibu Tawala Sichalwe.
Aidha Katibu Tawala Sichalwe amewataka watendaji ambao ni wabovu wawajibishwe haraka iwezekanavyo ili kuhakikisha hakuna mzaha katika utendaji kazi na utekekelezaji wa majukumu ya Serikali. Hata hivyo, ameagiza Watendaji Kata kuiitisha vikao vya haraka kwa Watumishi waliopo chini yao ikiwa na lengo la kukumbushana majukumu ya kiutendaji hasa katika ukusanyaji wa mapato.
Kwa upande wa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali Ndugu Raymond Mweli amesema katika utendaji kazi kumekuwa na baadhi wa Watendaji hawana umakini katika suala la ukusanyaji wa mapato na ndio wamekuwa kikwazo katika ukusanyaji wa mapato.
"Lack of seriousness (Kukosa umakini) kwa Watendaji wengi ndio unatuangusha" Amesema Ndugu Raymond huku akiendelea kusisitiza kuwa hata sita kuchukua hatua kwa Watendaji ambao wataonesha kukwamisha Maendeleo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.
Kikao hicho kimefanyika leo Disemba 16, 2025 kikiwakutanisha Katibu Tawala wa Wilaya ya Mbarali, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Wakuu wa Idara pamoja na Watendaji wa Kata zote za Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali.