13/05/2026
SERIKALI YATENGA SHILINGI BILIONI 171 KUTEKELEZA MIRADI YA TASHICO
Serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi imetenga jumla ya Shilingi bilioni 171 katika mwaka wa fedha 2026/27 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi na ukarabati wa meli chini ya Kampuni ya Meli Tanzania (TASHICO).
Akisoma Bajeti ya Wizara ya Uchukuzi bungeni mjini Dodoma leo tarehe 13.5.2026, Waziri wa Uchukuzi Prof. Makame Mbarawa alisema kuwa fedha hizo zitatumika kuimarisha usafiri wa njia ya maji katika maziwa makuu pamoja na kuongeza uwezo wa biashara na usafirishaji nchini.
"Fedha hizo zitaelekezwa katika utekelezaji wa miradi mikubwa ikiwemo ujenzi wa meli mpya ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 3,500 katika Ziwa Tanganyika pamoja na kuanza ujenzi wa meli mbili za mafuta zenye uwezo wa kubeba lita 600,000 kila moja katika ziwa hilo," Prof. Mbarawa alisema
Aidha, Serikali imepanga kuanza ujenzi wa meli mpya yenye uwezo wa kubeba abiria 600 na mizigo tani 400 katika Ziwa Tanganyika pamoja na meli mpya ya mizigo yenye uwezo wa kubeba tani 3,000 katika Ziwa Victoria.
Katika hatua nyingine, Serikali itaendelea kukamilisha upembuzi yakinifu utakaoiwezesha TASHICO kufanya biashara katika Bahari ya Hindi. Sambamba na hilo, Serikali imepanga kuendelea na ujenzi wa kiwanda cha kujengea meli katika Ziwa Tanganyika chenye uwezo wa kuhudumia meli zenye uzito wa tani 5,000.
Prof. Mbarawa alieleza kuwa miradi mingine itakayotekelezwa ni pamoja na ukarabati mkubwa wa meli ya MV. Mwongozo na kumalizia ukarabati wa meli ya MV. Liemba katika Ziwa Tanganyika ambayo ina asilimia 70 ya utekelezaji.
Pia, Serikali itaendelea na ukarabati wa meli za MT. Nyangumi na MV. Clarias katika Ziwa Victoria pamoja na ununuzi wa mabehewa ya kubeba mizigo kwa ajili ya meli ya MV. Umoja.
Miradi mingine iliyotajwa ni pamoja na ununuzi wa boti za uokoaji katika maziwa makuu, uboreshaji wa mifumo ya TEHAMA kwa ajili ya ukusanyaji wa mapato na ukarabati wa meli ya MV. Songea inayohudumia Ziwa Nyasa.
Hatua hiyo inaelezwa kuwa sehemu ya jitihada za Serikali za kuimarisha sekta ya usafiri wa majini nchini, kuongeza usalama wa usafiri na kuchochea ukuaji wa biashara na uchumi kupitia usafirishaji wa majini.