23/05/2026
THAMANI YA MAZAO YA NYUKI YAONGEZEKA, MAUZO YA ASALI YAFIKIA SH. BILIONI 19.2
TABORA, Mei 22, 2026, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema sekta ya ufugaji nyuki inaendelea kuongeza mchango wake katika uchumi wa Taifa huku thamani ya mazao ya nyuki ikiendelea kukua kutokana na ongezeko la uzalishaji na mauzo ya asali ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Nyuki Duniani yaliyofanyika katika Viwanja vya Kumbukumbu ya Vita mkoani Tabora, Dkt. Kijaji alisema ushiriki wa sekta binafsi unaendelea kuwa mhimili muhimu katika kuifanya Tanzania kuendelea kung’ara kimataifa katika sekta ya ufugaji nyuki.
Alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji, wadau wa maendeleo na sekta binafsi ili kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya nyuki, hatua itakayochochea ajira, kuongeza kipato cha wananchi na kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, mwaka 2025 Tanzania iliuza nje tani 1,596.8 za asali ikilinganishwa na tani 951 mwaka 2024, huku thamani ya mauzo hayo ikifikia Shilingi bilioni 19.2.
“Ndugu zangu, tunaona jinsi zao hili litokanalo na nyuki linavyoendelea kuongeza thamani kwa Taifa. Mbali na Tanzania kushika nafasi ya pili Afrika katika uzalishaji wa asali, thamani ya asali imepanda hadi kufikia Sh bilioni 19.2 mwaka jana. Hii ni hatua kubwa katika kuthamini mchango wa sekta ya nyuki,” alisema Dkt. Kijaji.
Aidha, alisema sekta ya ufugaji nyuki inakadiriwa kuajiri takribani watu milioni mbili nchini na imeendelea kuwa moja ya sekta zenye mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi.
Katika kuendeleza sekta hiyo, Dkt. Kijaji alisema Serikali inaendelea kutekeleza mpango wa “Achia Shoka, Tundika Mzinga” unaolenga kuongeza uzalishaji, ajira na ushiriki wa vijana katika shughuli za ufugaji nyuki.
Aliongeza kuwa Tanzania imeendelea kushika nafasi ya kwanza kwa uzalishaji wa asali katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kusini, ikiwa ya pili barani Afrika na ya 14 duniani.
Aidha, maadhimisho ya mwaka 2026 yanaongozwa na kaulimbiu isemayo “Uhifadhi wa Nyuki kwa Ustawi”, inayolenga kuhimiza uhifadhi wa mazingira, ustawi wa nyuki na maendeleo endelevu.