06/09/2026
MOROGORO KUMEKUCHA, MKWAWA RALLY 2026 YATIKISA
MOROGORO. Morogoro imeendelea kujijengea nafasi katika ramani ya michezo ya magari nchini baada ya Mkwawa Rally of Morogoro 2026 kufunguliwa rasmi, Septemba 5, huku Serikali ikiwataka wananchi kunufaika na fursa zinazotokana na mashindano hayo.
Mashindano hayo ya siku mbili, yanayofanyika katika maeneo ya Shamba la Miti Morogoro, yamefikia msimu wake wa pili na yamewakutanisha washiriki na wadau wa mchezo huo kutoka ndani na nje ya Tanzania.
Akifungua mashindano hayo, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, M***a Ramadhani Kilakala, alisema Serikali imejipanga kuhakikisha usalama wa washiriki na watazamaji wote, akisisitiza kuwa Morogoro ni eneo salama kwa matukio makubwa ya michezo.
Kilakala aliwakaribisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi, huku akiwataka wananchi kutumia uwepo wa mashindano hayo kuongeza kipato kupitia shughuli mbalimbali za biashara.
Mkuu huyo wa wilaya pia aliipongeza Tanzania Forest Services Agency (TFS) kwa kuendelea kuwa tayari kuandaa mazingira ya mashindano hayo kwa mwaka wa pili mfululizo, akisema hatua hiyo inasaidia kuitangaza Morogoro k**a eneo linaloweza kuandaa matukio makubwa ya michezo.
Kwa upande wake, Naibu Kamishna wa Uhifadhi DCC Dk. Hamza Kateti, aliwakaribisha washiriki na mashabiki katika Shamba la Miti Morogoro, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya waandaaji, TFS na wadau wa michezo katika kuendeleza michezo na utalii.
Kateti alisema TFS itaendelea kushirikiana na waandaaji ili kuhakikisha michezo inatumika pia kutangaza vivutio vya utalii na umuhimu wa uhifadhi.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuhitimishwa, Septemba 6, 2026, huku mashabiki wa mchezo wa magari wakisubiri kuona bingwa wa msimu huu.