03/06/2026
HOSPITALI YA RUFAA YA KANDA YA MBEYA (MZRH) NA MAMLAKA YA BANDARI TANZANIA (TPA) ZAINGIA MAKUBALIANO YA KUWAPATIA WAFANYAKAZI TPA HUDUMA ZA MATIBABU YA DARAJA LA JUU
Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Mbeya (MZRH) na Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) zimesaini rasmi makubaliano ya kutoa huduma za matibabu ya kibobezi na daraja la juu (VIP) kwa wafanyakazi wa mamlaka hiyo, huku hospitali ikitangaza mapinduzi makubwa ya kimatibabu yaliyolenga kuifanya kuwa kituo kikuu cha tiba utalii kwa nchi za SADC.
Hatua hiyo imefikiwa leo, Juni 3, 2026, baada ya pande zote mbili kuridhia na kusaini Hati ya Makubaliano (MoU) pamoja na Mkataba wa Kiwango cha Huduma (SLA). Nyaraka hizo zimesainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa MZRH, Dkt. Godlove Mbwanji, na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Bw. Plasduce Mkeli Mbosa mara baada ya kuwasilishwa na Mashaka Karume, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TPA.
Akizungumza katika hafla hiyo, iliyofanyika mapema leo katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji ameelezea kuwa ushirikiano huo ni sehemu ya mikakati ya hospitali hiyo kusogeza huduma za afya maeneo ya kazi, sambamba na kuonyesha maboresho makubwa ya kibingwa yaliyofanyika katika kuanzishwa kwa upasuaji wa moyo na kukaribia kukamilika kwa maabara ya kisasa ya uchunguzi wa mishipa ya damu (Cathlab), Kuimarika kwa huduma za upasuaji wa ubongo, moyo na mishipa ya fahamu pamoja huduma za kibingwa za kubadilisha na kupandikiza nyonga na magoti.
Kwa upande wake, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Ndg. Mashaka Karume, amebainisha kuwa mkataba huo unaenda kuleta mageuzi makubwa kiutendaji kwa kuondoa vikwazo vya kiafya vinavyowakabili wafanyakazi wa mamlaka hiyo, hasa wa Kanda ya Nyanda za Juu Kusini.