23/05/2026
Halmashauri ya Mji Makambako yazindua jukwaa la vijana
Na. Lina Sanga
Halmashauri ya Mji Makambako imezindua jukwaa rasmi la vijana (Vijana platform) ili kuwakutanisha vijana pamoja kujadili masuala mbalimbali kwa lengo la kujenga Taifa.
Akizungumza na vijana kabla ya kuzindua jukwaa hilo,Bi. Elice Simonile, Mkuu wa divisheni ya Maendeleo ya jamii Mkoa wa Njombe ambaye alikua Mgeni rasmi, amewapongeza vijana kwa kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa jukwaa hilo na kutoa hoja zenye mashiko zinazowahusu vijana ili zifanyiwe maboresho.
Pia, amewasisitiza vijana kulinda Amani ya nchi na kuhakikisha jukwaa hilo linakua muhimili mkuu wa kudumisha Amani kwani Serikali imeweka jitihada kubwa katika kuwawezesha vijana, hivyo ni wakati wa vijana kuingia ofisi yoyote ya Serikali na binafsi kujifunza masuala mbalimbali ili kuongeza ujuzi na ubunifu sambamba na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ili kutambua fursa zilizopo.
Ametoa wito kwa vijana kuwa na subira katika kupata huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Serikali, kwani kuna sharia na utaratibu wa utoaji wa fedha hizo na zinatolewa kwa foleni hivyo vijana watambue kuwa kuchelewa kupata sio makusudi ya Serikali bali ni suala la mfumo ambao Serikali imeweka ili fedha hizo ziwafikie walengwa.
Naye, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Makambako, Mhe. Robert Shejamabu amewataka vijana walioshiriki uzinduzi wa jukwaa hilo kujitofautisha na vijana wengine kwa kujitambua na kutambua walipotoka,kwani watoto wa wasaka tonge au mama ntilie ndiyo wanaoibadilisha dunia endapo watatambua wanataka nini na wafanye nini.
Awali,vijana walipata nafasi ya kuwasilisha hoja mbalimbali akiwemo Bw. Kemcho Kidava,Tyson Nziku na Neema Dononda waliiomba Serikali kupunguza bei ya pembejeo za kilimo ili kuwawezesha vijana kujiajiri kupitia kilimo,kutoa mikopo ya asilimia 10 kutolewa kwa wakati ili vijana waweze kutimiza malengo pamoja na kuendelea kutoa elimu ya uzalendo kwa vijana ili wawe na uelewa kabla ya kufanya maamuzi.
Uzinduzi huo umefanyika leo katika ukumbi wa Greencity sambamba na uzinduzi wa kongamano la vijana kuelekea siku ya mapokezi ya Mwenge wa Uhuru Mei 25, 2026.