06/06/2026
Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET), Dkt. Aneth Komba, amesema shindano la Taifa la Stadi za Ufundishaji la mwaka 2026 ni la nne kwa walimu wa elimu ya awali na msingi na la pili kwa walimu wa elimu ya sekondari, likihusisha halmashauri zote 184 za Tanzania Bara.
Ameyasema hayo leo Juni 6, 2026 katika hafla ya tuzo ya Taifa ya stadi za ufundishaji kwa walimu wa Awali, Msingi na Sekondari lililofanyika katika ukumbi wa maktaba mpya UDSM.
Amesema kwa upande wa elimu ya awali, shindano hilo limejikita katika kuimarisha umahiri wa ufundishaji wa stadi za kusoma, hususan sauti za herufi ambazo zimekuwa changamoto kwa baadhi ya wanafunzi katika kuzitamka na kuzitumia kwa usahihi katika kuunda silabi na maneno.
“Lengo la shindano hili ni kusaidia kutatua changamoto za ufundishaji na ujifunzaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (K*K) ili kuhakikisha wanafunzi wanazimudu stadi hizo muhimu wanapofikia Darasa la Tatu." Amesema
Ameeleza kuwa maandalizi ya shindano hilo yalihusisha uchambuzi wa matokeo ya wanafunzi kupitia taarifa za Baraza la Mitihani la Tanzania pamoja na maeneo mapya yaliyoingizwa katika mtaala ili kubaini maeneo yanayohitaji kupewa kipaumbele.
Kwa mujibu wa Dkt. Komba, walimu walitakiwa kuandaa andalio la somo, kujirekodi wakifundisha kwa muda wa dakika 10 hadi 15 na kupakia video pamoja na andalio hilo katika mfumo wa kidijitali wa National Teaching Skills Competition System kwa ajili ya tathmini.
Jumla ya walimu 3,153 walijisajili katika mfumo huo, huku walimu 1,263 sawa na asilimia 40 wakifanikiwa kupakia video zao kwa ajili ya tathmini katika ngazi ya halmashauri.
Amesema tathmini ilifanyika katika ngazi tatu ambazo ni halmashauri, mkoa na taifa kwa kuzingatia vigezo mbalimbali ikiwemo ubora wa maudhui, mtiririko wa somo, matumizi ya mbinu shirikishi, matumizi ya TEHAMA, matumizi ya zana za kufundishia, ukuzaji wa stadi za karne ya 21 na matumizi ya upimaji endelevu katika mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji.
Katika mchujo wa shindano hilo, video 751 zilifanikiwa kuingia ngazi ya mkoa kutoka video 1,263 zilizotathminiwa katika ngazi ya halmashauri. Kati ya hizo, video 232 zilichaguliwa kuingia ngazi ya taifa.