31/05/2026
📌SAMIA KALAMU AWARDS 2026 YAZINDULIWA RASMI
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) zimeanza maandalizi ya Tuzo za Uandishi wa Habari na Makala za Maendeleo (Samia Kalamu Awards - SKA) 2026 zikiwa na lengo la kuendelea kuhamasisha uzalishaji wa maudhui yenye ubora yanayochangia maendeleo ya Taifa.
Akizungumza Jumapili tarehe 31 Mei, 2026 jijini Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa mchakato wa kupokea kazi za kushindanishwa, Mwenyekiti wa SKA na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mhandisi Peter Mwasalyanda, amesema SKA ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuendelea kutambua mchango wa Waandishi wa Habari za maendeleo nchini.
Amesema tuzo hizo zinalenga kutambua, kuthamini na kuhamasisha uzalishaji wa maudhui ya ndani yenye ubora yanayochangia kuelimisha, kuhabarisha na kuburudisha, huku yakiimarisha taswira chanya ya Taifa kupitia habari za maendeleo.
Mwasalyanda amesema katika awamu ya kwanza ya tuzo hizo kulikuwa na mwitikio mkubwa kutoka kwa wadau wa sekta ya habari wakiwemo taasisi za habari, Waandishi wa Habari binafsi, watengenezaji wa maudhui mtandaoni na Maafisa Habari wa Serikali.
Taarifa zaidi kuhusu SKA 2026 zinapatikana kwenye tovuti ya samiaawards.tz au kupitia kiunganishi hiki https://samiaawards.tz/