10/09/2026
Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), tarehe 9 Septemba 2026, imekutana na Chama cha Madereva wa Taksi Mtandao Tanzania (TODA), Wamiliki wa Mifumo ya Taksi Mtandao pamoja na wadau wengine, wakiwemo kampuni zinazojihusisha na uuzaji wa magari yanayotumia nishati safi. Kikao hicho kimefanyika katika Ofisi za LATRA Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma za Taksi Mtandao nchini na kuhakikisha huduma hiyo inapatikana kwa ufanisi wakati wa mashindano ya AFCON 2027 katika miji ya Dar es Salaam, Arusha na maeneo ya jirani.
Akifungua kikao hicho, Bw. Salum Pazzy, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano - LATRA, amewataka wadau hao kuwa mfano wa kuigwa katika utoaji wa huduma ya Taksi Mtadao kwa wateja wao, kwa kuzingatia ubora, usalama na ufanisi wa huduma hiyo, hususan katika kipindi hiki na wakati wa mashindano ya AFCON 2027.
Kwa upande wake, Bw. Patel Ngereza, Kaimu Meneja Udhibiti Magari ya Abiria - LATRA, amewasihi wadau hao kupanua wigo wa utoaji wa huduma za Taksi Mtandao katika mikoa mingine nchini ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi kunufaika na huduma hiyo.
Aidha, Bw. Ngereza amewataka wadau hao kuimarisha mifumo ya usalama ili kuhakikisha abiria wanapotumia huduma za Taksi Mtandao wanakuwa na uhakika na usalama wa safari zao. Vilevile, amewataka wadau kuhakikisha wanakuwa na uelewa wa pamoja kati ya Madereva na Wamiliki wa Mifumo ya Taksi Mtandao kuhusu masuala ya kamisheni pamoja na ofa zinazotolewa na wamiliki wa mifumo hiyo kwa abiria ili kuepusha migogoro inayoibuka baina yao.
Wadau waliohudhuria kikao hicho kwa pamoja wameipongeza LATRA kwa kuandaa kikao hicho, wakieleza kuwa ni hatua muhimu yenye lengo la kujenga ushirikiano na kuboresha zaidi utoaji wa huduma za Taksi Mtandao nchini.