25/07/2017
Mafanikio na changamoto za matumizi ya TEHAMA katika masuala ya haki za binadamu.
Tume ya haki za binadamu na utawala bora nchini Tanzania inazidi kufanya kazi zake kwa kujiimarisha kutokana na maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano TEHAMA nchini Tanzania na duniani kwa ujumla.
Katika kuzidi kujiimarisha tume ya haki za binadamu na utawala bora tarehe 11 mwezi Aprili, 2017, ilikutana na waandishi wa habari na wawakilishi wa vikundi mbalimbali ili kuwapa elimu ya haki za binadamu na utawala bora waandishi wa habari na kuwashauri watumie weledi wao katika kuripoti na kuandika taarifa zao kwa jicho la haki za binadamu
Katika semina/warsha hiyo iliyofunguliwa na kamishina wa haki za binadamu na Utawala bora Salma Ali Hassan mambo mengi yalijadiliwa lakini kubwa zaidi ilikuwa nafasi ya vyombo vya habari katika kuelimisha umma wa watanzania kuhusiana na haki za binadamu.
Wakati akifungua warsha hiyo iliyofanyika jijini Mwanza , kamishina wa tume hiyo Salma Ali Hassan alisema kuwa ni wazi kuwa waandishi wa habari, wapiga picha na watengenezaji wa vipindi mara nyingi wamekuwa wakiweka wazi masahibu wanayopata watu k**a kudhalilishwa na kuonewa na watu wengine. Hivyo, aliwataka waandishi wa habari kutumia weledi na umakini wao katika kuyaripoti na kuyaandika masahibu hayo
Mafanikio ya TEHAMA katika masuala ya haki za binadamu
Ikiwa tume hiyo sasa inajiweka karibu na vyombo vya habari , lakini pia kutokana na maendeleo ya teknolojia ya habari na mwasiliano TEHAMA,masuala muhimu ya haki za watu katika jamii yetu yaliweza kujadiliwa na washiriki.
Maendeleo ya TEHAMA yamekuja na mabadiliko mengi katika kusaidia utoaji wa taarifa za masuala ya haki za binadamu nchini Tanzania. Kwa mfano, tukio la mwaka jana 2016 la mwanafunzi aliyeshambuliwa na walimu mkoani Mbeya liliweza kurekodiwa kwa kutumia simu ya mkononi jambo lilisababisha taarifa zile kusambaa nchi nzima.
Lakini pia maendeleo ya TEHAMA yamekuwa na mchango mkubwa sana katika usalama wa watu kwa njia ya mitandao. Kutokana na maendeleo ya TEHAMA nchini Tanzania watu mbalimbali wamekuwa wakitumia uhuru wao na haki yao ya kujieleza na kutoa maoni yao kwa kutumia mitandao ya kijamii. Yote haya yanaifannya Tume ya haki za binadamu na utawala bora nchini Tanzania kuwa karibu na watanzania kwa kupata taarifa nyingi zinazohusiana na masuala ya haki za binadamu na utawala bora.
Mbali na hilo, kutokana na kuimarika kwa teknolojia ya habari na mawasiliano tume ya haki za binadamu pia imekuwa ikipokea malalamiko mbalimbali kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi yaani SMS kwa namba 0754 460259. Kwa kutumia mfumo huu, tume imekuwa ikipokea malalamiko mbalimbali na kuyafanyia kazi kwa mujibu wa taratibu za uendeshaji wake.
Lakini pia katika warsha iliyofanyika jijini Mwanza , waandishi wa habari walifundishwa kuhusu Human Rights Based Approach(HRBA) ambayo inawataka waandishi wa habari kuzingatia haki za binadamu katika kila habari wanayoandika na wanayoripoti.
Katika uwasilishaji wake Bwana Albert Kakenki alisema kwa kutumia dhana ya HRBA waandishi wa habari wanatakiwa wazingatie maeneo matatu muhimu ambayo ni nia ya kuandika habari(goal), mchakato wa kuandika habari(process) na matokeo yanayotegemewa baada ya habari kuandikwa au kuripotiwa (outcome).
Baada ya uwasilishaji wake bwana kakenki alisema kuwa tume sasa hivi inajitahidi kutoa semina mbalimbali kwa waandishi wa habari katika kanda na mikoa mbalimbali ili kuzingatia haki za binadamu kwa namna habari zinavyoandikwa na kuripotiwa
Changamoto za TEHAMA katika masuala ya haki za binadamu
Katika masuala ya haki za binadamu kumekuwa na matukio mengi yanayoashiria changamoto za TEHAMA katika kuripoti matukio haya. Mengi ya matukio haya ni yale ya uvunjifu wa haki za binadamu kutokana na maendeleo ya TEHAMA hasa kwa kutumia simu za mkononi za kupangusa(smartphones)
Kwanza, kumekuwa na usambazaji wa picha za watu waliokufa kwa ajali mbaya . picha hizi zimekuwa hazizingatii haki ya wanaozitazama kwa sababu si kila mtu ana uwezo wa kuangalia picha za mtu aliyekufa kwa ajali mbaya huku zikitoa kabisa utu (dignity)
Pili, kumekuwa na uingiliaji wa faragha za watu (privacy) kwa kuingilia uhuru wa mtu na maisha yake binafsi. Haya yamekuwa yakifanyika kwa watu kupiga picha au kurekodi sauti za watu bila ridhaa yao na kuvunja haki yao ya faragha ambayo inatambulika kikatiba.
Tatu, kumekuwa na udakaji (hacking) wa taarifa za watu kwa kutumia simu za kupangusa(smartphone) jambo ambalo pia limekuwa likiingilia uhuru wa mtu katika kuwa na taarifa zake. Hii inahatarisha hadi usalama wa taarifa za watu katika barua pepe yaani e-mail zao.
Nne, kumekuwa na utoaji wa taarifa za uchochezi (seditious information) kwa kutumia simu za mkononi ni kuondoa haki za upande mmoja unaolemewa. Haya yamesababisha hadi baadhi ya watu kukumbwa na adhabu kutokana na sheria ya makosa ya kimtandao ya mwaka 2016 yaani Cyber Crime Act of 2016
Hatimaye washiriki na waandishi wa habari katika warsha hiyo walipata nafasi ya kuuliza maswali ambayo yalijibiwa na maafisa mbalimbali wa tume wakiwemo wanasheria na viongozi. Miongoni mwa mambo yaliyozua mjadala ni uhuru wa chombo hicho kilichoanzishwa kwa sheria na. 7 ya mwaka 2001 ambapo maelezo yaliyotolewa ni kuwa kwa mujibu wa sheria hiyo tume ya haki za binadamu ni chombo huru japo iko chini ya ofisi ya rais.
Mwisho
Chanzo: Semina ya tume ya haki za binadamu na utawala bora Mwanza
Imeandikwa na Yohani Gwangway