30/04/2026
WATUMISHI TVLA WATAKIWA KUONGEZA BIDII NA UBUNIFU
Na Daudi Nyingo
Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), Dkt. Stella Bitanyi, amewataka watumishi wa TVLA kufanya kazi kwa bidii, weledi na mshikamano ili kuendeleza mafanikio yaliyopo, akisisitiza kuwa maendeleo ya TVLA yanategemea uwajibikaji wa kila mtumishi pamoja na kujivunia nafasi zao ndani ya taasisi.
Dkt. Bitanyi alitoa kauli hiyo Aprili 28, 2026, wakati wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TVLA kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa TVLA, Temeke jijini Dar es Salaam.
Alisema TVLA imejipanga kuimarisha mazingira ya kazi ili kuongeza tija, akibainisha kuwa tayari kila kituo kimepatiwa gari jipya kwa ajili ya kurahisisha utekelezaji wa majukumu, huku mipango ikiendelea ya kuboresha maabara ili ziendane na teknolojia ya kisasa.
“Ni muhimu kila mtumishi kuwa na nidhamu na bidii ya kazi, na kuhakikisha anaiwakilisha vyema TVLA popote anapokuwa. Sote tunapaswa kutambua kuwa hii ni taasisi kubwa yenye mchango wa moja kwa moja katika ustawi wa sekta ya mifugo na uchumi wa Taifa. Hivyo, kila mmoja akitimiza wajibu wake ipasavyo, TVLA itasonga mbele kwa kasi zaidi,” alisema Dkt. Bitanyi.
Sambamba na hilo, aliwataka watumishi kujikita katika tafiti za kisayansi, hususan katika shughuli za maabara, akieleza kuwa tafiti ni chachu ya ubunifu na msingi wa utoaji wa huduma bora.
Katika hatua nyingine, Dkt. Bitanyi alisema TVLA ina mkakati wa kuimarisha uzalishaji wa chanjo za mifugo ili kukidhi mahitaji ya ndani na hata soko la kimataifa, hatua inayotarajiwa kuongeza mchango wa taasisi katika maendeleo ya sekta ya mifugo.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/2026 pamoja na rasimu ya bajeti ya 2026/2027, Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mipango, Masoko na Habari, Bw. Prosper Haule, alisema kuwa hadi kufikia Machi 2026, TVLA imezalisha dozi milioni 107.59 za chanjo za mifugo.
Sambamba na hilo TVLA inaendelea na ujenzi wa kituo cha kanda ya kati mkoani Dodoma, pamoja na kuboresha miundombinu ya usafiri kwa kununua magari matatu. Aidha, imekarabati nyumba za watumishi katika vituo vya Tanga na Mwanza, huku ikiendeleza shamba la mifugo la Mivumoni Tanga na kuimarisha shughuli za utafiti pamoja na ununuzi wa vifaa vya maabara.
Kuhusu rasimu ya bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027, alisema vipaumbele ni pamoja na kuongeza uzalishaji wa chanjo, kuendelea na ujenzi wa maabara, pamoja na kujenga ukuta kuzunguka Taasisi ya Chanjo Tanzania (TVI) iliyopo Kibaha.
Vipaumbele vingine ni kuendelea na ujenzi wa kituo cha TVLA kanda ya kati Dodoma, ukarabati wa Maabara Kuu ya Mifugo (CVL), ununuzi wa magari mawili, pamoja na upatikanaji wa kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa maabara na ofisi katika kituo cha Kigoma.
Wakizungumza katika kikao hicho, viongozi wa TUGHE akiwemo Mwakilishi wa TUGHE Taifa, Bw. Haruna Migeyo, Mjumbe wa Baraza Kuu TUGHE Serikalini, Bw. Benjamin Bikulamchi, pamoja na Katibu wa TUGHE Mkoa wa Dar es Salaam, Bi. Jamila Semang'anda waliupongeza uongozi wa TVLA kwa utekelezaji mzuri wa majukumu yake.
Walisema mafanikio hayo yanaakisi utekelezaji wa falsafa ya 4R za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, zinazojikita katika Maridhiano, Ustahimilivu, Mageuzi na Kujenga upya Taifa.
MWISHO