30/05/2026
Menejimenti ya TCAA Yatembelea Mradi wa Ujenzi wa Majengo ya CATC
Menejimenti ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) ikiongozwa na Mkurugenzi Mkuu, Dkt. Jabiri K. Bakari, imetembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa Majengo ya Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) uliopo njia panda ya Banana jijini Dar es Salaam, Mei 30, 2026.
Lengo la ziara hiyo lilikuwa kujionea hatua za utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati kwa maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini. Ziara hiyo pia ni sehemu ya juhudi za uongozi wa Mamlaka kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Bakari alisema uongozi wa TCAA unaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati, kwa ubora unaotakiwa na kwa kuzingatia viwango vya kitaalamu na kimataifa.
Alisema kukamilika kwa ujenzi wa majengo ya Chuo cha CATC kutakuwa na mchango mkubwa katika kuendeleza rasilimali watu wenye ujuzi wa kitaalamu katika sekta ya anga sambamba na kupunguza utegemezi wa mafunzo ya nje ya nchi.
"Mradi huu ni muhimu sana kwa maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini. Hakikisheni kuwa utekelezaji wake unazingatia ubora, ratiba na viwango vya kimataifa," amesema Dkt. Bakari.
Kwa upande wake, Meneja Mradi kutoka TCAA Mhandisi Stephen Mwakasasa alisema ujenzi unaendelea kulingana na michoro na usanifu uliokubaliwa huku usimamizi wa karibu ukiendelea kufanyika ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora uliopangwa.
Ziara hiyo pia iliwezesha Menejimenti ya TCAA kupata maelezo kuhusu hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa mradi, changamoto zilizopo na mikakati ya kuendelea kuboresha utekelezaji wake hadi kukamilika.
Kukamilika kwa mradi wa ujenzi wa Chuo cha Usafiri wa Anga kunatarajiwa kuongeza uwezo wa taifa katika kutoa mafunzo ya kitaalamu ya anga na kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini kwa kuzingatia viwango vya kimataifa.
Mradi huo wa miaka mitatu unatekelezwa na kampuni ya CRJE kutoka nchini China.