07/06/2024
KWANINI UOMBEE FAMILIA YAKO!.
Zaburi 127:1
''BWANA asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. BWANA asipoulinda mji Yeye aulindaye akesha bure. ''
Kibiblia neno nyumba linasimama k**a mbadala wa neno familia, ndoa, ukoo au jengo la mahali ambako watu wanaishi,
Mfano,
Mwanzo 20:18
''Maana BWANA alikuwa ameyafunga matumbo ya watu wa NYUMBANI mwa Abimeleki, wasizae, kwa ajili ya Sara mkewe Ibrahimu.''
· KWANINI UOMBEE FAMILIA YAKO.
01. Familia inaweza ikabeba adhabu kwa sababu ya makosa ya mmoja kutoka katika familia hiyo.
Mwanzo 20:18
''Maana BWANA alikuwa ameyafunga matumbo ya watu wa nyumbani mwa Abimeleki, wasizae, kwa ajili ya Sara mkewe Ibrahimu.''
Familia ya Abimeleki yote yaani wote wa jamaa yake alioishi nao matumbo yao ya uzazi yalifungwa ili wasipate kuzaa kwa sababu tu ya kosa la Abimeleki kumchukua mke wa IBRAHIM akitaka kumuoa.
Je familia yenu au ukoo wenu unapata adhabu gani, na
Je ni kosa la nani?.
Mpendwa yaimarishe magoti yako kwaajili ya familia yako, maana kwa kukosekana mtu anayesimama kwaajili ya familia yenu ndiko kunakoifanya familia iyumbe.
Ezekieli 22:30-31
"Nami nikatafuta mtu miongoni mwao, atakayelitengeneza boma, na kusimama mbele zangu mahali palipobomoka, kwa ajili ya nchi, nisije nikaiharibu, lakini sikuona mtu.
Kwa sababu hiyo nimemwaga ghadhabu yangu juu yao; nimewateketeza kwa moto wa hasira yangu; nami nimeileta njia yao wenyewe juu ya vichwa vyao, asema Bwana MUNGU.
02. MUNGU anaweza kuizingira familia kwa sababu ya ucha MUNGU wa kiongozi wa familia.
Ayubu 1:10
''Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na NYUMBA yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi.''
Ayubu k**a kiongozi wa familia alikuwa mcha MUNGU, na
Kwasababu ya ucha Mungu wake familia ilizungukwa na ukigo wa Mungu.
Ukiona ucha MUNGU umesababisha kuzingirwa na MUNGU basi ujue kwamba kuna familia au viongozi wa familia sio wacha MUNGU hivyo hakuna kuzingirwa na MUNGU ndio maana majanga hayaishi.
Ukiokoka wewe na ukajitambua, kiroho wewe unakuwa lango la familia na kiroho unakuwa kiongozi wa familia au ukoo hivyo familia yako wanaweza kukaa salama kwa maombi yako.
03. Nyumba/ukoo/familia inaweza kubeba laana.
Mithali 3:33
''Laana ya BWANA i katika nyumba ya waovu, Bali huibariki maskani ya mwenye haki.''
Inawezekana unatokea familia iliyolaaniwa labda kwa sababu kiongozi wa familia alimwaga damu ya mtu asiye na hatia.
Inawezekana unatokea ukoo uliolaaniwa kwa sababu ya maovu mabaya yaliyokithiri kwa watu wanaotokea ukoo huo.
Wewe uliyepata neema ya kuokolewa na Bwana YESU inakupasa sana kujinasua kwenye laana za ukoo au familia au nyumba maana usipojua kuomba unaweza hata wewe ukashikiliwa na laana hiyo hiyo.
Daudi alikuwa ameokoka kuliko hata wewe, alikuwa muombaji kuliko wewe na alikuwa mtumishi wa MUNGU,
lakini ikulu au ofisi aliyoirithi ilikuwa na adhabu kwa sababu ya makosa ya mtangulizi wake,
Madhara ya adhabu ya ofisi hiyo yalimpata hadi Daudi ambaye hakuhusika katika kosa hilo,
2 Samweli 21:1
''Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; naye Daudi akautafuta uso wa BWANA. BWANA akasema, Ni kwa ajili ya Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni.''
Jifunze kuombea familia, nyumba au nafasi unayoiingia kuirithi baada ya alikuwepo kuondoka,
· Inawezekana Nafasi/ofisi yako ina laana hivyo hata anayeingia hapo laana inaambatana naye, Rafiki jitambue na omba ili kujiondoa kwenye agano/laana ya familia, ukoo au nyumba.
· Kuna nyumba zimejengwa juu ya ardhi iliyobeba laana hivyo lazima ujue kuomba ili kujitenga na laana iliyo katika ardhi kwa ajili ya watakaojenga juu yake.
Yoshua 6:26
''Naye Yoshua akawaapisha kiapo wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za BWANA mtu yule atakayeinuka na kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake kwa kufiliwa na mzaliwa wa kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na mtoto wake mwanamume aliye mdogo.''
Vipi k**a unakaa katika ardhi ambayo kila mtoto wa kwanza kuzaliwa lazima afe?
Ndugu, unahitaji sana kuomba juu ya familia, nyumba au ukoo na ardhi yake.
04. Familia inaweza kubarikiwa na MUNGU kwa sababu ya uwepo wa Mtumishi wa MUNGU anayeishi maisha matakatifu.
Mwanzo 39:5
''Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, Bwana akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa Bwana ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba.''
Hizi ni dondoo chache kwaajili ya kukujengea msukumo wa kuombea familia yako.
Kristo Yesu na akusaidie kulielewa hili.