01/09/2026
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Jamhuri ya Watu wa China waanza majadiliano ya kina yaliyolenga kukamilisha upatikanaji wa hati ya makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Hospitali mpya ya moyo nchini.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya, Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na Jamhuri ya Watu wa China kukutana na kupitia vipengele mbalimbali vya makubaliano vinavyohusu ujenzi wa hospitali hiyo pamoja na maeneo mengine ya ushirikiano katika sekta ya afya.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Mkurugenzi wa Idara ya Tiba kutoka Wizara ya Afya Dkt. Hamad Nyembea alisema majadiliano hayo yanalenga kuhakikisha kuwa pande zote mbili zinafikia uelewa wa pamoja kuhusu vipengele vya makubaliano kabla ya hatua ya kusaini hati.
“Tumekutana na wataalamu wenzetu kutoka Jamhuri ya Watu wa China kupitia na kujadili baadhi ya vipengele vya hati ya makubaliano ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Hospitali mpya ya moyo pamoja na miradi mingine iliyopo chini ya Sekta ya Afya, tunaamini kwamba kupitia majadiliano haya tutakamilisha taratibu za makubaliano na kuanza utekelezaji”, alisema Dkt. Nyembea.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Dkt. Angela Muhozya alisema JKCI itatoa ushirikiano wa kutosha kwa wataalamu kutoka Jamhuri ya Watu wa China wakati wote wa kutekeleza mradi huo.
“Tutahakikisha kabla ya yote tunawatambulisha katika mazingira yetu, taratibu na mifumo yetu pamoja na kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa karibu na wataalamu wetu ili lengo tulilokusudia liweze kufanikiwa”, alisema Dkt. Angela.
Naye Mshauri wa Masuala ya Uchumi na Biashara katika Ubalozi wa China nchini Tanzania Chu Kun alisema Jamhuri ya Watu wa China inafahamu umuhimu wa ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo mbili.
“Tumeshaanza kupitia baadhi ya vipengele vya makubaliano tukiwa na lengo moja la kuwezesha ujenzi wa hospitali hii mpya ya moyo hapa Tanzania ili kuwasaidia wagonjwa wa moyo kupata huduma hapa nchini”, alisema Chu.