31/05/2026
MHESHIMIWA BALOZI SWAHIBA MNDEME AFANYA MKUTANO NA WATANZANIA WAISHIO SWEDEN (DIASPORA)
Mheshimiwa Balozi Swahiba Mndeme amefanya mkutano na Watanzania waishio nchini Sweden tarehe 30 Mei 2026 katika viwanja vya Ofisi ya Ubalozi wa Tanzania jijini Stockholm.
Lengo la mkutano huo lilikuwa kwa Balozi Swahiba kufahamiana na Wanadiaspora, kujadili mipango na mikakati ya Nchi ya kimaendeleo, kujadilia masuala ya Diaspora na kuwasilisha salamu za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Katika Mkutano huo, Balozi Swahiba alieleza vipaumbele vya Serikali atakavyovisimamia wakati wa utekelezaji wa majukumu yake ya Balozi wa Tanzania Nchini Sweden na katika nchi zingine atakazoziwakilisha ambazo ni Denmark, Norway, Finland, Iceland, Estonia, Latvia, Lithuania na Ukraine. Aidha, Balozi Swahiba alibainisha kuwa moja ya vipaumbele vyake ni kuimarisha ushiriki wa Diaspora katika maendeleo ya Tanzania kwa kutumia ujuzi, maarifa na uzoefu wao.
Vilevile aliahidi kuendelea kutoa kipaumbele kwa kukuza na kueneza matumizi ya lugha ya Kiswahili katika eneo la uwakilishi wake, hususan kwa kuwezesha upatikanaji wa vitabu na vifaa vya kufundishia lugha hiyo.
Aidha, Alisisitiza umuhimu wa Watanzania waishio nje ya nchi kutumia ushawishi wao katika kukuza biashara, kuvutia uwekezaji nchini na kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania.
Balozi Swahiba pia, aliwahimiza wanadiaspora kuendelea kuwa na mshikamano na kuunganisha nguvu zao kupitia chombo kimoja kitakachorahisisha uratibu wa masuala yao. Pia aliwataka kuendelea kuisemea vyema Tanzania na kudumisha uzalendo ili kuendeleza taswira chanya ya nchi katika ngazi ya kikanda na kimataifa.
Wakati wa Mkutano huo masuala mbalimbali yanayohusu diaspora ikiwemo suala la Hadhi Maalum, sheria ya mirathi kwa wanadiaspora pale wazazi au ndugu zao wanapofariki dunia nchini, huduma mbalimbali za Kikonseli yalijadiliwa.
Mheshimiwa Balozi aliwahimiza wanadiaspora kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali zinazoratibiwa na Ubalozi, ikiwemo maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani yatakayofanyika mwezi Julai 2026 pamoja na Serengeti Bonanza, litakalofanyika jijini Stockholm mwezi Agosti 2026.