27/11/2014
THE MOMBASA REPUBLICAN COUNCIL
(MRC)
P.O. BOX 81510 MOMBASA
EMAIL: [email protected]
27th. November, 2014.
TAARIFA YA KUTANGAZA TAREHE YA KOTINI.
Ndugu Wazalendo wa Pwani hamjambo? Tuamkeni; k**a mnavyo juwa Vuguvugu letu la The Mombasa Republican Council (MRC), tunafuata sheria ndiyo maana tukapeleka kesi zetu zote mahak**ani. Kunayo kesi yetu moja al-maarufu kesi ya IEBC kesi ambayo tuliish*taki IEBC na vitengo vingine tisa (9) vya serikali vinavyofanya kazi zake pasipo kufuata utaratibu wa sheria yaani kimaonevu, kuwaonea watu hasa wa Pwani, hivyo basi tumeitisha kura ya maoni (referendum) hapa Pwani kwenye kesi hiyo, lengo haswa nikujitoa kwenye minyororo ya wakoloni weusi wanaotukandamiza sawasawa na tulivyokuwa sisi wa Pwani hapo karne za 15, 16, 17, 18 na hata zaidi ya nusu ya karne ya 19 Waingereza walipo peana uhuru Kenya na wakatuchanganya pamoja ili tupate kulindwa kwa vile Kenya watakuwa na serikali kamili, tukadhania eti tutapumzika shida kumbe tunaruka matope tunakanyaga kinyesi. Hivi sasa kesi iliyo mbele yetu ni ile ya IEBC inayosikizwa (Hearing) tarehe 17th December 2014. Wapwani wazalendo, k**a tujuavyo hatuna wafadhili wakutufadhili na shughuli hizi zetu isipokuwa wafadhili ni sisi wenyewe na hivi sasa Mawakili wetu wanahitaji pesa za kugharamia kesi zetu, Enyi wapwani, tuendelee kufuata mtindo aliokuwa akiufanya Baba yetu Baba wa Wapwani mkombozi wetu na shujaa wa Pwani Hayati Ronald Gideon Ngala. Baba yetu huyu alikuwa wakati anafanya shughuli za ukombozi, huitisha michango, nao wapwani kwa uzalendo wao walikuwa wakimchangishia kwa kima akitakacho na akaendeleza shughuli pasipo na kudeteleka huku wala kule. Mpaka ilipofika wakati wa kuiteremsha bendera ya Sultan hapa Pwani, Wapwani wazalendo walifanya kazi ya ziada, wakamchangishia Baba yetu Ronald Ngala akiwa Uingereza kwenye mikutano ya Lancaster House, wakampelekea kukohuko naye kwa heshima yake akamkabidhi pesa hizo kiongozi waliyekuwa wamempisha mbele kuongoza Kenya (Hayati Mzee Jomo Kenyatta) apeane kwa Sultan wa Zanzibar. Pesa hizo ndizo zilizopelekea kuandikwa kwa mikataba hapo mwaka 1963 na hata kuiteremsha bendera ya Sultan hapa Pwani. Basi tunawaomba wapwani sote tuige mfano uohuo na wala tusichoke kwani kupata uhuru sio kazi rahisi wala ndogo.
TAHADHARI.
Tahadhari hii tumeitoa kwa wapwani wazalendo tutahadharini dhidi ya wapwani wenzetu na wanaopata shida k**a sisi tunavyozipata, lakini lakushangaza nikwamba, wapwani wawahawa wanazunguka wakieneza uongo na uvumi usiokuwa na faida yoyote kwa Mpwani ila kumrudisha nyuma mpwani. Propaganda za kuwapotosha wapwani eti mambo yamekwisha, sasa hivi tutapatiwa nchi yetu kwani Wazungu wameshakuja tayari kutupatia nchi yetu. Huu ni uongo na ni njia moja au nyengine ya kumlemaza akili Mpwani aone ugumu wa kuchangisha pesa, hizi ni propaganda potofu na wala hazifai kuketi kwenye akili zetu haswa kwetu sisi jamii ya Pwani. Hawa ni watu wanaotumiwa na maadui zetu wasiotaka kumuona Mpwani akifurahia matunda ya uhuru wake. Watu k**a hawa tunafaa kuwakemea k**a shetani anavyo kemewa na kulaaniwa. Sisi k**a viongozi, tumeketi na kulizungumzia jambo hili na hivi sasa tumepitisha kuwafuatilia watu hawa, mmoja baada ya mwengine na k**a mnavyofahamu sisi kila kitu chetu tunakifuatilia kisheria, sisi tumeshaanzisha uchunguzi wetu dhidi ya watu hawa, pindi tutakapokamilisha uchunguzi wetu, basi watu hawa wajue watakiona cha mtema kuni. Sisi tutawaandama na mkono wa sheria mpaka tuhakikishe wamefika mbele za sheria na wajieleze na kujitambulisha mbele ya watu wa Pwani na mahak**a endapo nyadhifa hizo za kukutana na wafadhili wa Umoja wa Mataifa (UN) kuifadhili MRC na Wapwani kwa jumla walizipata vipi. Itakuwaje k**a kweli ni wafadhili wa MRC kusiwe hata kiongozi mmoja aliyekutana na wafadhili hao? Hayo yote ni maneno ya kufitinisha, basi watu hao tunawajuwa mmoja baada ya mwengine, tunawafuatilia na shughuli zao kila wanapopitia ili tukamilishe uchunguzi wetu. Kila siku wanawadanganya watu tarehe Fulani tutapatiwa nchi yetu na siku zinakuja zikipita watu hawa ni waongo, wanafiki, wachochezi, wafitini wa kutufitinisha sisi wenyewe kwa wenyewe tutofautiane mwisho tuanze kukosana na kuteta ambapo Serikali ndivyo inavyotaka, mwisho wapange njama za kutuuwa. Sisi nasi kwakuwa tumegonganishwa tuanze kuonyeshana vidole wenyewe kwa wenyewe na hata kupelekea kuhasiriana ambapo adui huyo wetu ndio atapata nguvu zaidi kulilemaza jambo letu. K**a mnavyojuwa kunazo njia nyingi za kusafiri; kwa ndege, gari, meli, baisikeli na hata kwa miguu, sisi wenyewe mwendo wetu ni kwa miguu, tusimkubalie mtu yeyote mwenye nia ya kutushika nguo akituregesha nyuma ama kututembeza kwa kifua. Kwa hivyo Wapwani Wazalendo tuwe na subra tusikubali mtu yeyote kututowa kwenye timing ya sheria na tukajiingiza kwenye mitego isiyokuwa mipango yetu, kwa sababu waswahili husema kikulacho kinguoni mwako, basi tusipo kuwa waangalifu kwa jambo hili tutalitia michanga sisi wenyewe kupitia kwa hao maadui wetu wakitutumia sisi wenyewe, “ASHINDWE PEPO”. Ndugu zetu Wapwani, tujue yakwamba kilicho na mwanzo, hakikosi mwisho na Mwenyezi Mungu ndiye mwenye kujuwa kilakitu hata mwisho wa ukombozi wa nchi yetu. Kwa hivyo tuendelee kumuomba Mwenyezi Mungu kwa kila jambo letu na kumuomba azidi kutupatia “SUBRA”. Sisi viongozi wenu tunapitia wakati mgumu na mitihani mingi sana lakini tuko na subra kwani tunajuwa jambo hili ni lazima liwe na mitihani ya kiaina yake na nilazima pia tuivumilie tukimtegemea Mwenyezi Mungu, nanyinyi pia mtuonee huruma na mtuombee Mola wetu atuzidishie subra tuliyonayo na tuzidi kusonga mbele kuzipigania haki zetu za Wapwani kwa kutumia sheria mpaka tutakapo zitia mikononi haki hizi na kujitawala wenyewe.
Mwisho tujue yakwamba, hakuna mtu yeyote atakaye toka nje ya Pwani atuonee huruma na kutuleta kuwa kitu kimoja pasipo, kubaguana sisi kwa sisi kidini, rangi na kikabila ila ni sisi viongozi wa MRC tukishirikiana na viongozi wa mashinani na wafuasi sote k**a kitu kimoja ndiposa tulishinde “JINAMIZI” hili lililo tukalia na kutukandamiza bila hata ya huruma. Ushirikiano ni kitu bora.
“EWE MWENYEZI MUNGU, IBARIKIE PWANI NA UTUBARIKIE PIA SISI WA PWANI, UTUFUNGULIE MLANGO WAKUONA VILE TULIVYO TAWANYWA NA MAADUI ZETU, UTUONDOSHEE KILA AINA YA BALAA HAPA KWETU PWANI, WANAOTUDHULUMU HAKI ZETU UWAONYESHE NJIA YA KUTUTENDEA HAKI, UTUPATIE AMANI NDANI YA NCHI YETU YA PWANI, UWAADHIRISHE WANAFIKI WOTE WANAOENDA KINYUME NA HATA WALE WATAKAO ENDA KINYUME CHA VIONGOZI WETU WA MRC, UWAONGEZEE NGUVU, MAARIFA NA MSHIKAMANO VIONGOZI WETU WA MRC, TUZIPATE HAKI ZETU, TUIKOMBOE NCHI YETU YA PWANI NA TUISHI KWA AMANI, AMIN !!!
“UNITED WE STAND, DIVIDED WE FALL”.