10/07/2022
WARIOBA,KABUDI, NA HARAKATI ZA KATIBA MPYA..
KWA UFUPI
Jaji Warioba na wajumbe wenzake, Profesa Palamagamba Kabudi, Joseph Butiku, Hamphrey Polepole, Mwantumu Malale na Awadh Ali Said walitoa ufafanuzi huo katika mdahalo la Katiba lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere jana.
Dar es Salaam. Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba na wajumbe wa tume hiyo, jana walitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali kuhusu mchakato wa Katiba katika mjadala uliofanyika hapa kiasi cha kuwafanya waliohudhuria siyo tu kumshangilia, bali walimsindikiza hadi alipoingia kwenye gari lake na wakilifuata na kulisukuma.
Jaji Warioba na wajumbe wenzake, Profesa Palamagamba Kabudi, Joseph Butiku, Hamphrey Polepole, Mwantumu Malale na Awadh Ali Said walitoa ufafanuzi huo katika mdahalo la Katiba lililoandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere jana.
Jaji Warioba ndiye alianza kuzungumza kwa kukanusha madai yaliyotolewa juzi katika mdahalo mwingine, kuwa amepeleka maoni mapya serikalini.
Alisema madai hayo hayana ukweli bali maoni aliyowasilisha serikalini yalitokana na maoni ya wananchi waliyokusanya wakati wakiandaa Rasimu ya Kwanza ya Katiba ambayo yataweza kusaidia katika kuandaa Katiba ya Tanganyika.
Juzi, katika mdahalo uliorushwa na Star TV, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi alidai kuwa Jaji Warioba amewasilisha serikalini maoni mapya, ukiacha yale ambayo yapo katika Rasimu ya Katiba.
Jaji Warioba alisema Tume iliandaa sura ya kwanza iliyohusu mali na maliasili na sura ya tano kuhusu Serikali ya Muungano na sura ya nne iliyoelezea serikali za mitaa.
“Sura ya nne na tano tulibaki nazo lakini Machi 27, mwaka huu niliandika barua kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Chikawe (Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe) kwa kuwa alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria kipindi hicho na nikawakabidhi ili isaidie katika mchakato wa Katiba hasa wakati wa kuandaa Katiba ya Tanganyika,” alisema Jaj