04/09/2026
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mha. Benedict Ndomba, amewataka wanafunzi wanaofanya mafunzo kwa vitendo katika Kituo cha Utafiti, Ubunifu na Uendelezaji wa Jitihada za Serikali Mtandao (e-GovRIDC), kutumia ipasavyo fursa hiyo kwa kujenga maarifa, ujuzi na uwezo wa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira.
Mha. Ndomba ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na wanafunzi hao waliopata fursa ya kufanya mafunzo kwa vitendo katika kituo hicho kwa kipindi cha wiki 10.
Amesema mafunzo kwa vitendo ni sehemu muhimu katika kuwaandaa wanafunzi kwa mazingira halisi ya kazi, kwa kuwa yanawawezesha kuunganisha maarifa wanayoyapata darasani na ujuzi wa vitendo, hususan katika sekta ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Kwa upande wake, Meneja wa Utawala na Rasilimali Watu wa e-GA, Jafari Maganga, amewataka wanafunzi hao kuzingatia kanuni, taratibu na maadili ya Utumishi wa Umma wakati wote wa mafunzo yao.
Naye Meneja wa e-GovRIDC, Dkt. Jaha Mvula, amesema ushiriki wa wanafunzi katika miradi hiyo unalenga kuwapatia uzoefu wa vitendo, kuwawezesha kutumia maarifa waliyoyapata katika masomo yao na kuwajengea uwezo wa kushiriki katika ubunifu na utatuzi wa changamoto za kiteknolojia.
Kwa niaba ya wanafunzi wenzake, Leticia Omari kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST), ameishukuru e-GA kwa kuwapatia fursa hiyo, akisema mafunzo hayo yatawasaidia kuongeza maarifa, ujuzi na uzoefu wa mazingira halisi ya kazi.
Kituo hicho kimepokea jumla ya wanafunzi 62 kutoka vyuo vikuu 10 kwa ajili ya mafunzo kwa vitendo ya kipindi cha wiki 10. Wanafunzi hao wamegawanywa katika makundi mbalimbali yanayoshiriki katika utekelezaji wa jumla ya miradi 14 inayohusisha maeneo tofauti ya teknolojia ya TEHAMA.