Wizara ya Fedha

Wizara ya Fedha Ukurasa Rasmi wa Wizara ya Fedha Tanzania.

Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati za Ukaguzi wa Ndani wa Serikali, wanaendelea na Mafunzo yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha...
18/09/2026

Wenyeviti na Wajumbe wa Kamati za Ukaguzi wa Ndani wa Serikali, wanaendelea na Mafunzo yaliyoandaliwa na Wizara ya Fedha kwa lengo la kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao ya usimamizi, ushauri na ufuatiliaji wa utendaji wa Idara/vitengo vya ukaguzi wa ndani na mifumo ya udhibiti wa ndani katika taasisi za Serikali.

Katika mafunzo hayo wawezeshaji wameendelea kutoa mafunzo mbalimbali ikiwemo, maadili ya ukaguzi, namna ya kuchambua taarifa za mali za taasisi na kuhoji mabadiliko ya thamani ya mali ili kuhakikisha taarifa zinazowasilishwa zinaakisi hali halisi.

Mafunzo hayo yanayoendelea kufanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Wizara ya Fedha, ya kuimarisha mifumo ya ukaguzi wa ndani na Kamati za Ukaguzi wa ndani k**a sehemu ya juhudi za kuongeza uwazi, uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali za Serikali.

Serikali imewataka wafanyabiashara, wawekezaji na taasisi za fedha nchini kutumia fursa zilizopo katika uchumi wa Tanzan...
17/09/2026

Serikali imewataka wafanyabiashara, wawekezaji na taasisi za fedha nchini kutumia fursa zilizopo katika uchumi wa Tanzania kuwekeza mitaji katika sekta za uzalishaji, miundombinu, teknolojia na biashara ili kuongeza ajira, uzalishaji na ushindani wa Tanzania katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Mhandisi Mshamu Ali Munde (Mb), alipokuwa akizungumza katika Jukwaa la Viongozi wakuu wa Makampuni Binafsi (The 200 CEOs Business Forum Fouth Edition), uliofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency, jijini Dar es Salaam, ambapo amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji maamuzi madhubuti ya uwekezaji kutoka serikalini na sekta binafsi.

Mhe. Munde alisema Tanzania inalenga kujenga uchumi jumuishi, wenye ustawi, haki na kujitegemea, unaoongozwa na sekta binafsi na wenye ushindani, huku ikilenga kufikia uchumi wa takribani Dola za Marekani trilioni moja na kipato cha wastani cha zaidi ya Dola za Marekani 7,000 kwa mtu kwa mwaka ifikapo mwaka 2050.

“Utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, unaenda sambamba na Mpango wa Muda Mrefu wa Maendeleo wa 2026/27–2050/51 pamoja na mipango ya miaka mitano ya maendeleo, ikiwemo Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV) wa 2026/27–2030/31, ambapo msingi muhimu wa utekelezaji wa mipango hii ni mfumo wa uwekezaji wa asilimia 70 kwa asilimia 30, na sekta binafsi inatarajiwa kuchangia sehemu kubwa ya uwekezaji huku Serikali tukiendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisera, kisheria, kitaasisi na kiuchumi” alisema Mhe. Munde.

Alisema kuwa, pamoja na umuhimu wa uwekezaji wa moja kwa moja kutoka nje (FDI) kutokana na mchango wake katika kuleta mitaji, teknolojia, utaalamu na fursa za masoko ya kimataifa, Serikali pia inalenga kuwawezesha Watanzania kushiriki zaidi katika uwekezaji ndani ya nchi na itaendelea kuunga mkono ushiriki mpana katika hati fungani za Serikali, mifuko ya uwekezaji wa pamoja, dhamana za kampuni pamoja na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Mhe. Munde aliwataka viongozi wa kampuni, wawekezaji na taasisi za fedha kutumia fursa hiyo ya mitaji kwa kuwekeza katika sekta zinazoongeza uzalishaji na thamani ya uchumi.

“Nawataka kuelekeza mitaji katika sekta za uzalishaji, kujenga minyororo imara ya thamani ndani ya nchi na ukanda wa Afrika Mashariki, kutumia teknolojia na akili unde (Artificial Intelligence) kwa uwajibikaji, kuwekeza katika ujuzi na ubunifu pamoja na kujenga kampuni za Kitanzania zinazoweza kushindana katika masoko ya Afrika na dunia” alisema Mhe. Munde.

Aidha aliwahakikishia Serikali iko tayari kusikiliza, kushirikiana na kuendelea kuboresha mazingira ambayo biashara zinaweza kustawi, na mabadiliko yanayolengwa kupitia Dira ya Taifa 2050 yatategemea ubora wa maamuzi yanayofanywa na muhimu zaidi uwezo wa kuyageuza maamuzi hayo kuwa uwekezaji, uzalishaji, ajira na ustawi wa pamoja.

Alisema kuwa Serikali imeendelea kutekeleza mageuzi ya kiuchumi, kisheria, kitaasisi na kiutawala yenye lengo la kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini, ambapo awamu ya kwanza ya Mpango wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (MKUMBI I) iliyoanzishwa mwaka 2018, ilisaidia kurahisisha taratibu za biashara, kuimarisha huduma kwa wawekezaji na kupunguza vikwazo vya udhibiti, huku ikiendelea na awamu nyingine ya mageuzi hayo ili kukidhi mahitaji ya sasa ya kiuchumi, kiteknolojia na kibiashara.

Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Mhe. Dkt. Pius Chaya, alisema kuwa Serikali itaendelea kuwawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kupitia sera zake ili kupata vyanzo mbalimbali vya fedha kwa ajili ya kukuza na kupanua biashara zao.

Mhe. Chaya alisema kuwa, Serikali inahitaji kuona biashara zikikua kutoka ndogo kuwa za kati, kutoka za kati kuwa kampuni kubwa, na hatimaye kutoka kampuni zinazofanya kazi ndani ya nchi kuwa kampuni imara zinazoweza kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.

Amesisitiza kuwa Serikali ina jukumu la kuweka mazingira wezeshi, huku sekta binafsi ikiwa na wajibu wa kujenga taasisi imara, kuimarisha utawala bora wa kampuni, kuwekeza katika watu na teknolojia, na kujenga biashara zenye uwezo wa kushindana nje ya mipaka ya Tanzania.

“Tanzania iko katika nafasi nzuri kunufaika kutokana na utulivu wa kisiasa, jiografia yake ya kimkakati, rasilimali za asili, ongezeko la idadi ya vijana, maboresho ya miundombinu pamoja na fursa zinazotokana na masoko ya kikanda na bara” alisema Mhe. Dkt. Chaya

Aidha, aliitaka sekta binafsi kutumia fursa hizo kwa kuangalia zaidi ya soko la ndani, huku Serikali ikiendelea kushirikiana na wafanyabiashara kubaini na kuondoa changamoto zinazokwamisha uwekezaji na ukuaji wa biashara.

“majukwaa k**a haya yanapaswa kwenda zaidi ya kuwa sehemu za mazungumzo na kujenga mitandao, bali yazalishe matokeo yanayoonekana katika uchumi, ikiwemo kuunganisha mtaji na fursa halisi za uwekezaji, kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi na kubaini vikwazo vinavyoathiri uwekezaji na ukuaji wa biashara” alisema Mhe. Dkt. Chaya

Wizara ya Fedha imeendesha mafunzo kwa wajumbe na wenyeviti wa Kamati za Ukaguzi wa Ndani kwa lengo la kuwajengea uwezo ...
17/09/2026

Wizara ya Fedha imeendesha mafunzo kwa wajumbe na wenyeviti wa Kamati za Ukaguzi wa Ndani kwa lengo la kuwajengea uwezo katika kutekeleza majukumu yao ya usimamizi, ushauri na ufuatiliaji wa utendaji wa Idara/vitengo vya ukaguzi wa ndani na mifumo ya udhibiti wa ndani katika taasisi za Serikali.

Akizungumza wakati wa kufungua Mafunzo hayo, Kaimu Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha, Mhandisi Kenneth Nindie, alisema mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha wajumbe kuelewa kwa kina wajibu wao katika kuhakikisha shughuli za ukaguzi wa ndani zinafanyika kwa ufanisi, weledi na kwa kuzingatia misingi ya maadili ya taaluma.

Alitoa rai kwa k**ati hiyo kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, weledi, uhuru na uwajibikaji ili kuimarisha mfumo wa usimamizi wa rasilimali na udhibiti wa ndani Serikalini.

‘’Nawahimiza kutekeleza majukumu yenu inavyopaswa kwa kuzingatia nidhamu pia kuhakikisha vikao vinafanyika kwa mujibu wa ratiba, wajumbe wanapata taarifa muhimu kwa wakati na wanajiandaa kabla ya vikao” Alisema Mhandisi Nindie.

Aliwataka wajumbe wa k**ati hiyo kuendelea kuongeza weledi na kutumia teknolojia katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuongeza ufanisi na matokeo chanya katika kazi za ukaguzi, kwa kuwa matumizi ya teknolojia ni miongoni mwa hatua muhimu za kuboresha utendaji wa shughuli za ukaguzi.

Alisema mabadiliko ya teknolojia yanaendelea kuathiri namna kazi za ukaguzi zinavyotekelezwa, hivyo ni muhimu kwa wakaguzi kuendana na mabadiliko hayo na kuhakikisha wanakuwa na ujuzi unaohitajika katika mazingira ya sasa ya kazi.

Awali, akimkaribisha Kaimu Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha, Mhandisi Kenneth Nindie, Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali Msaidizi, Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Paison Mwamnyasi, aliwataka washiriki wa mafunzo hayo kuyazingatia kwa umakini ili kufikia lengo lililokusudiwa la mafunzo hayo.

‘’Mafunzo haya yana umuhimu sana kwenye utendaji wetu hivyo ni muhimu kuyazingatia ili kuleta matokeo Chanya yaliyolengwa na Wizara’’ alisema Bw. Mwamnyasi.

Naye Mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Mkaguzi wa Ndani Mwandamizi kutoka Idara ya Mkaguzi Mkuu wa Ndani wa Serikali, Wizara ya Fedha, Bw. Andrew Nicholaus, alieleza kuwa Kamati ya Ukaguzi ina jukumu muhimu la kusaidia mamlaka inayoteua katika kutekeleza wajibu wake wa usimamizi, huku ikitakiwa kubaki huru katika kutoa ushauri na uangalizi.

Mafunzo hayo yanayoendelea kufanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), ni sehemu ya utekelezaji wa dhamira ya Wizara ya Fedha, ya kuimarisha mifumo ya ukaguzi wa ndani na Kamati za Ukaguzi wa ndani k**a sehemu ya juhudi za kuongeza uwazi, uwajibikaji na matumizi sahihi ya rasilimali za Serikali.

Wizara ya Fedha imeendelea kuandaa na kuboresha miongozo mbalimbali inayolenga kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya uka...
16/09/2026

Wizara ya Fedha imeendelea kuandaa na kuboresha miongozo mbalimbali inayolenga kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya ukaguzi na kuongeza ufanisi wa kazi hiyo, ili kuendelea kulinda fedha za umma na kukuza uchumi wa nchi.

Hayo yameelezwa na Kaimu Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali, Wizara ya Fedha, Mhandisi Kenneth Nindie, wakati akifungua Mafunzo ya Uelewa na Ugawaji wa Mwongozo wa Ukaguzi wa Mifumo ya Taarifa kwa Wakaguzi wa Ndani wa Serikali, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mabele jijini Dodoma.

Mhandisi Nindie alisema kuwa mwongozo huo unahusisha hatua mbalimbali za mchakato wa ukaguzi, na kwamba baadhi ya vipengele vyake vinapitia hatua ya uhakiki ili kuhakikisha vinaendana na mahitaji na viwango vinavyotakiwa.

"Tunachukua baadhi ya vipengele kwa ajili ya kuvithibitisha, ambapo ni muhimu kupitia na kuthibitisha miongozo hiyo kabla ya kuanza kutumika kikamilifu. alisema Mhandisi Nindie.

Alieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuhakikisha kuwa miongozo inayotumika katika kazi za ukaguzi ina ubora, inaeleweka na inawasaidia watendaji kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa watumishi kuwa na vyeti vya kitaaluma (certification), kwakuwa hatua hiyo ni muhimu katika kuongeza ufanisi na ubora wa utekelezaji wa majukumu yao.

"Suala la kuwa na vyeti vya kitaaluma limekuwa sehemu muhimu ya mipango ya kuimarisha uwezo wa watumishi. Natambua kuwa tangu mwaka 2021 kulikuwa na mpango uliolenga kuongeza idadi ya watumishi wenye vyeti hivyo," alisema Mhandisi Nindie.

Alibainisha kuwa kuendelea kuwekeza katika ujuzi na taaluma za watumishi ni hatua muhimu katika kuboresha utendaji kazi na kuhakikisha majukumu ya taasisi yanatekelezwa kwa viwango vinavyohitajika.

Mafunzo hayo yaliandaliwa na Wizara ya Fedha, kupitia Idara ya Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali yakiwakutanisha Wakaguzi wa Ndani kutoka taasisi za umma na kutoka Wizara ya Fedha, ili kuwaongezea uelewa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar, ameongoza ujumbe wa Tanzania, akiambatana na Waziri wa Mawasiliano na Te...
13/09/2026

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar, ameongoza ujumbe wa Tanzania, akiambatana na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki katika mkutano na watendaji wa kampuni ya POSCO International jijini Seoul Jamhuri ya Korea Kusini ambapo pamoja na mambo mengine, wamejadili namna ya kuendeleza fursa za uwekezaji wa kimkakati katika sekta za madini, nishati, na kilimo.

Mkutano huo umesisitiza dhamira ya pamoja ya kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kuifanya Tanzania kuwa kituo kikuu cha shughuli za POSCO barani Afrika.

Majadiliano yalijikita katika maendeleo ya mradi wa grafiti wa Mahenge, ambao kwa sasa uko katika hatua ya mwisho ya ongezeko la mtaji na unatarajiwa kukamilika mwaka huu.

Pande zote mbili zimekubaliana kuhusu umuhimu wa miradi muhimu ya miundombinu, ikiwemo ujenzi wa barabara na ununuzi wa mabehewa ya reli, ili kuunga mkono mnyororo wa thamani wa madini. Miradi hii inatekelezwa kwa ushirikiano na Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi (EDCF) na Benki ya Exim ya Korea.

Mbali na mradi wa Mahenge, ujumbe wa Tanzania umewasilisha mpango mpana wa ushirikiano uliopanuliwa ikiwemo kuongeza thamani ya madini, kuendeleza viwanda vya kusindika nikeli, kobalti, na shaba, hasa katika mkoa wa Dodoma.

Miradi mingine iliyopendekezwa ni pamoja na uwekezaji katika uzalishaji wa mafuta ya mawese, utengenezaji wa mbegu ili kupunguza utegemezi wa uagizaji, na usimamizi wa mashamba makubwa, ubunifu wa kidijitali na viwanda, kushirikiana katika akili unde (AI) ya viwandani, roboti, na uchambuzi wa kidijitali.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais Mtendaji wa POSCO international, Bw. Jae Sung Lim, ameitaja Tanzania k**a mmoja wa washirika wao watano wakuu wa kimkakati barani Afrika na Ili kurahisisha uhusiano huo unaokua, Kampuni hiyo imetangaza mipango ya kuanzisha ofisi ya uwakilishi nchini Tanzania, ikihama kutoka muundo wa sasa wa usimamizi unaoendeshwa kutoka Afrika Kusini.

Mkutano huo ulihitimishwa kwa pande zote mbili kukubaliana kudumisha mawasiliano ya karibu kupitia njia za kidiplomasia, ikiwemo Ubalozi wa Tanzania mjini Seoul, ili kuhakikisha utekelezaji wa haraka wa mipango hiyo ya kimkakati.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), ameongoza Ujumbe wa Tanzania kutembelea Chuo Kikuu cha Hanyang ERIC...
12/09/2026

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), ameongoza Ujumbe wa Tanzania kutembelea Chuo Kikuu cha Hanyang ERICA, jijini Seoul nchini Korea Kusini, pembezoni mwa Mkutano wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na nchi za Afrika, KOAFEC, akiambatana na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki (Mb).

Mhe. Balozi Omar, alitoa hotuba fupi ya shukrani, na kusisitiza kuwa Tanzania imejipanga kuendeleza ushirikiano kati yake na Chuo hicho.

Aidha, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Kairuki (Mb), kwa upande wake alisisitiza kuwa ziara yao katika Chuo Kikuu cha Hanyang ERICA ni hatua ya kimkakati ya kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu kufuatia ziara za awali za viongozi wa Tanzania nchini humo.

Alieleza kuwa matumizi ya akili unde (AI) na mabadiliko ya kidijitali ambayo Chuo hicho imekuwa ikifundisha ni nguzo kuu za maendeleo ya Tanzania, na Serikali inalenga kuimarisha ujuzi wa vijana, miundombinu ya data, na mifumo ya uvumbuzi kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050

Mhe. Kairuki alitoa mapendekezo tisa mahususi ya ushirikiano, yakilenga kuanzia utiaji saini wa MOU, kubadilishana wanafunzi, mafunzo ya wahadhiri, hadi kuanzishwa kwa Kituo cha Pamoja cha Utafiti (Korea-Tanzania Digital Innovation Lab).

Alionesha imani yake kuwa ERICA ina uwezo wa kutekeleza mapendekezo hayo na alisisitiza umuhimu wa kuona matokeo ya haraka, k**a vile mafunzo ya rasilimali watu, ujenzi wa maabara, na kuanzishwa kwa kampuni changa (startups).

Alihitimisha kwa kutoa mwaliko rasmi kwa Makamu wa Rais wa ERICA, Baek D**g-hyun, na ujumbe wake kutembelea Tanzania (Dodoma, Dar es Salaam, na Zanzibar) ili kuona fursa na utayari wa nchi katika kutumia fursa mbalimbali za uwekezaji unaopatikana nchini katika sekta mbalimbali.

Katika mkutano huo, Makamu wa Rais wa Chuo hicho Prof. D**g Baek, alijibu mapendekezo ya Mhe. Waziri Kairuki, akisema ni ya busara na muhimu.

Alikiri kuwa baadhi ya mapendekezo hayo yanaweza kutekelezwa kwa urahisi kwa sababu Serikali ya Korea tayari imetenga fedha kwa ajili ya ushirikiano na Tanzania, hivyo hakutakuwa na changamoto kubwa katika kuyaendesha.

Prof. Baek aliahidi kuwa Chuo kitayapitia mapendekezo hayo kwa kina ili kutafuta njia bora za kuyafanikisha.

Chuo Kikuu cha Hanyang ERICA ni Chuo kinachozingatia sana utafiti na teknolojia, hasa katika nyanja za AI, data science, robotics, cybersecurity, na semiconductors, Kina mfano wa kipekee wa elimu unaoitwa ICPBL (Industry-Coupled Problem-Based Learning) na mifumo ya kisasa ya kujifunza kwa masafa na kinafanya kazi kwa karibu na viwanda na sekta ya teknolojia, kikiwa na miundombinu k**a Campus Innovation Park na Ansan Science Valley.

Aidha, Chuo hicho kinafahamika k**a mfano wa kimataifa wa jinsi elimu, utafiti, na viwanda vinavyoweza kukua pamoja, na kina uwezo wa kutoa mafunzo ya hali ya juu na kinafanya ushirikiano na vyuo vingine vya kimataifa.

Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa inaendelea kuimarisha vyanzo vyake vya ndani vya fedha pamoja na matumizi ya mfumo wa...
12/09/2026

Serikali ya Tanzania imeeleza kuwa inaendelea kuimarisha vyanzo vyake vya ndani vya fedha pamoja na matumizi ya mfumo wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) katika kugharamia miradi ya maendeleo, ikisisitiza kuwa mikopo ya Serikali itaelekezwa katika miradi yenye manufaa ya muda mrefu kiuchumi na kijamii.

Hayo yalisemwa na Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), wakati wa mdahalo ulioongozwa na Mtaalamu wa Idara ya Hazina ya Marekani, Bw. Eric Meyer, kuhusu vyanzo vya fedha kwa ajili ya kuendeleza Sekta ya Afya, wakati wa Jukwaa la Mazungumzo ya Ngazi za Juu la Mawaziri wa Fedha, lililofanyika Nairobi, Kenya.

Mhe. Luswetula, aliyemwakilisha Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar katika mkutano huo, alisisitiza umuhimu wa Ubia kati ya Serikali na Sekta Binafsi (PPP) kuwa moja ya njia muhimu za kuongeza upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

“Tanzania iko tayari kushirikiana na sekta binafsi kupitia mikataba ya muda mrefu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali. Tunakaribisha kampuni na wawekezaji kushirikiana na Serikali katika uwekezaji wenye tija,” alisema Mhe. Luswetula.

Alisema Sera ya Serikali inalenga kukuza uwekezaji, kuongeza shughuli za kiuchumi na kuhakikisha sekta binafsi inapata nafasi kubwa zaidi katika kuchochea maendeleo ya Taifa.

Vilevile, Mhe. Luswetula alisema Serikali inatumia ushuru wa bidhaa (excise duty) k**a moja ya njia za kulinda afya za wananchi dhidi ya athari hasi zinazoweza kusababishwa na baadhi ya bidhaa, huku mapato yatokanayo na kodi hiyo yakisaidia kugharamia huduma na miundombinu ya afya.

Alisema ukusanyaji wa mapato kupitia kodi hizo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuongeza uwezo wa ndani wa kugharamia huduma za kijamii na kupanua wigo wa mapato ya Taifa.

Akizungumzia suala la mikopo, Mhe. Luswetula alisema Serikali haitumii mikopo bila kuzingatia uwezo wa miradi husika kuzalisha manufaa ya muda mrefu na kuchangia katika ulipaji wa madeni.

Alisema kipaumbele kinatolewa kwa miradi ya kimkakati, ikiwemo miundombinu ya msingi na uwekezaji mwingine wa mitaji wenye manufaa ya muda mrefu kwa uchumi na jamii.

“Hatutaki kukopa kwa sababu tu tunataka kupata fedha. Tunakopa pale ambapo uwekezaji una manufaa ya muda mrefu na tuna uhakika wa namna ya kurejesha deni,” alisema Mhe. Luswetula.

Alisema utaratibu huo unalenga kuhakikisha kuwa mikopo ya Serikali inatumika kwa nidhamu na kuelekezwa katika miradi inayoweza kutoa matokeo yanayostahili gharama ya fedha hizo.

Mhe. Luswetula alisema Tanzania inaendelea kutoka katika mfumo wa kutegemea zaidi fedha za wafadhili na kuelekea katika mfumo unaochanganya rasilimali za ndani, ufadhili wa pamoja na uwekezaji wa sekta binafsi.

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), amesema kuwa Tanzania na Korea Kusini zimekubaliana kuongeza kasi y...
11/09/2026

Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), amesema kuwa Tanzania na Korea Kusini zimekubaliana kuongeza kasi ya utekelezaji wa ahadi iliyotelewa na nchi hiyo ya dola za Marekani bilioni 2.5 kwa Tanzania kwa ajili ya kutekeleza miradi muhimu ya kimkakati itakayochochea maendeleo na ukuaji wa uchumi wa nchi katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu ya usafirishaji, teknolojia, utamaduni, viwanda na afya.

Mhe. Balozi Omar amesema hayo jijini Seoul, Korea Kusini, pembezoni mwa Mkutano wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Korea na nchi za Afrika, KOAFEC, wakati alipoongoza ujumbe wa Tanzania katika Mkutano huo pamoja na Benki ya Exim ya Korea ambayo ni wakala wa ukelezaji wa mfuko wa ushirikiano wa maendeleo ya kiuchumi wa Korea (EDCF).

Alisema Tanzania inathamini ushirikiano wa maendeleo wa Korea, lakini alisisitiza haja ya kuboresha utekelezaji wa miradi iliyokubaliwa kwa pamoja chini ya mfuko wa EDCF, akibainisha kuwa ucheleweshaji kwa upande wowote unaweza kudhoofisha ahadi zilizotolewa.

Alitoa wito wa uratibu wa karibu zaidi na juhudi madhubuti za kushughulikia ucheleweshaji katika utekelezaji wa miradi, tafiti za upembuzi yakinifu, na usanifu wa kina wa kihandisi, ambapo alisema baadhi ya miradi imechukua miaka kadhaa kabla ya kuanza kutekelezwa.

Mazungumzo hayo yamefanyika kufuatia mkutano wa Mawaziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Afrika na Korea, ambapo pamoja na mambo mengine, walijadili ushirikiano katika eneo la akili Unde (AI) kwa ajili ya maendeleo ya Bara la Afrika.

Akizungumzia matokeo ya Mkutano huo, Mhe. Balozi Omar amebainisha kuwa pande zote mbili zimekubaliana kufuatilia kwa karibu miradi iliyoahidiwa katika ziara ya Rais Dkt. Samia mwaka 2024 nhini Korea Kusini, ikiwemo mradi wa kwanza unaotarajiwa kuanza utekelezaji wake hivi karibuni wa ujenzi wa Chuo Mahiri cha Tehama jijini Dodoma.

Miradi mingine iliyojadiliwa na kupatiwa ufumbuzi ni pamoja na:Ujenzi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano na Maonesho Zanzibar, Ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni na mradi wa Uendelezaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Aliutaja mradi mwingine kuwa ni Ujenzi wa barabara ya Ifakara kuelekea Mahenge, inayohusiana na mradi wa uchimbaji wa madini ya graphite.

Kuhusu mradi wa ununuzi wa mabehewa ya treni kwa ajili ya reli ya SGR, pande zote mbili zimekubaliana kufanya mapitio ya pamoja ya gharama na wigo wa mradi ili kuhakikisha unatekelezeka kwa ufanisi.

Mazungumzo hayo yamehitimishwa kwa pande zote mbili kuahidi ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha miradi yote iliyokubaliwa inakamilika kwa wakati.

Kwa upande wake, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angelah Kairuki, alisema kuwa kupitia Mkutano huo Tanzania imenadi fursa mbalimbali za uwekezaji katika teknolojia bunifu zitakazo chochea ukuaji wa uchumi wa nchi na kukuza ajira na mapato ya Serikali kupitia kodi.

Aliwakaribisha wekezaji wa Korea, wafanyabiashara wa Korea wanaojihusisha na masuala ya teknolojia pamoja na teknolojia nyingine za kidijitali, kuja kuwekeza Tanzania katika uwekezaji wa miundombinu ya kidijitali. Ikiwemo vituo vya kutunzia taarifa (data centers), kukuza na kupanua mtandao wa mawasiliano wa 5G, kukuza upatikanaji wa fiber, ujenzi wa miundombinu ya mawasiliano ikiwemo minara ya mawasiliano.

“Lakini pia nimewakaribisha kuwekeza katika sekta ya Serikali Mtandao, kuja kuona namna gani huduma muhimu wanaweza kushirikiana na wakala wetu wa Serikali mtandao na Wizara, kuboresha huduma mbalimbali zinazotolewa na kiserikali, hizo za kijamii, za kielimu, za afya na huduma nyingine mbalimbali kupitia mifumo ya kidijitali” alisema Mhe. Kairuki

Alisema kuwa amewakaribisha pia kuwekeza katika teknolojia mbalimbali zikiwemo fedha, afya na utabibu, teknolojia za kuweza kusaidia uzalishaji katika kilimo na mnyororo mzima wa thamani.

Mhe. Kairuki pia aligusia suala la upatikanaji wa mtaji kwa ajili ya Shirika la Mawasiliano la Taifa (TTCL), uwekezaji katika fiber, maduka ya TTCL na huduma za simu ambapo wawekezaji wameonyesha nia ya kuwekeza na kushirikiana na Tanzania.

“Kama tunavyofahamu Tanzania tumejaliwa kuwa na idadi kubwa ya vijana na tunachokitaka kutumia idadi hiyo ya wingi wa vijana wetu kuwa ni faida kwa Taifa, faida kwa uchumi. Na hiyo ndiyo dhamira na azma kubwa ya Mheshimiwa Rais kupitia Serikali anayoiongoza ya awamu ya 6 kuona namna gani tunachochea fursa hizo kuja nchini na ziweze kutoa ajira kwa wananchi wetu”. Aliongeza Mhe. Kairuki.

Katika Jukwaa la KOAFEC la Mwaka huu lililobeba kaulimbiu ya “Harnessing AI and Digital Infrastructure for Africa's Transformation” uliandaliwa na Wizara ya Fedha na Uchumi ya Korea, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Korea Eximbank, uliwakutanisha Mawaziri wa Afrika wanaoshughulikia uchumi, fedha, Akioi Unde (Artificial Intelligence) na mageuzi ya kidijitali; viongozi wa AfDB; kampuni za Afrika; na washirika wa marndeleo wa kimataifa.

Lengo kuu la kukutana ni kujadiliana namna ya kutumia Akili Unde (Artificial Intelligence) na miundombinu ya kidijitali kuharakisha maendeleo ya Afrika kwa kuangazia uwekezaji, ufadhili wa maendeleo, ubunifu wa teknolojia na kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Korea na nchi za Afrika.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), amewakaribisha wawekezaji kuwekeza katika sekta ya afya Tanzania, ak...
11/09/2026

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), amewakaribisha wawekezaji kuwekeza katika sekta ya afya Tanzania, akisema nchi ina sera thabiti zinazotabirika pamoja na mazingira salama na rafiki kwa uwekezaji.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis M***a Omar (Mb), Mhe. Luswetula ametoa mwaliko huo wakati akichangia hoja katika Jukwaa la Mazungumzo ya Ngazi za Juu la Mawaziri wa Fedha kuhusu kuimarisha uwekezaji wa pamoja katika sekta ya afya, lililofanyika katika Hoteli ya JW Marriott, Nairobi, Kenya.

“Tanzania ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya afya, pamoja na sera imara na zinazotabirika zinazoambatana na mazingira bora ya uwekezaji na usalama. Kinachohitajika ni kufuata sheria za nchi ili uwekezaji uwe na manufaa kwa mwekezaji na Watanzania kwa ujumla,” alisema Mhe. Luswetula

Akizungumzia mkutano huo Mhe. Luswetula alisema majadiliano katika jukwaa hilo yalilenga kujadili mikakati ya kuongeza mapato ya ndani kwa ajili ya kugharamia huduma za afya, utekelezaji wa ahadi za pamoja za ufadhili pamoja na kuweka sera na mazingira wezeshi yatakayochochea uwekezaji katika sekta hiyo.

Alisema kuwa Tanzania imepiga hatua katika kuweka mazingira yanayowezesha upatikanaji na utoaji wa huduma bora za afya, hatua ambayo inatoa fursa zaidi kwa sekta binafsi kushiriki katika maendeleo ya sekta hiyo.

Aidha, alisema Tanzania imeendelea na utekelezaji wa programu ya Bima ya Afya kwa Wote, huku Serikali ikiwekeza kwa kiasi kikubwa katika eneo hilo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya nchini.

Alisema uwepo wa mfumo mpana wa bima ya afya unatarajiwa kuwa na mchango katika kuimarisha upatikanaji wa huduma za afya na kuwawezesha wananchi kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa shughuli zao za maendeleo.

Vilevile alisema kuwa majadiliano hayo yalihusu matumizi ya mbinu bunifu za ufadhili na mifumo ya kuchanganya vyanzo mbalimbali vya fedha ili kuongeza rasilimali zinazohitajika katika kuboresha huduma za afya.

Mkutano huo uliowakutanisha Mawaziri wa Fedha kutoka nchi mbalimbali za Afrika zilizosaini Hati za Makubaliano (MoU) na Serikali ya Marekani kuhusu ufadhili wa sekta ya afya ulihudhuriwa pia na Naibu Katibu wa Hazina ya Marekani anayeshughulikia Masuala ya Kimataifa, Bi. Erin Browne, pamoja na viongozi na maafisa mbalimbali kutoka nchi shiriki.

Tanzania na Marekani zimeeleza dhamira ya kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo...
11/09/2026

Tanzania na Marekani zimeeleza dhamira ya kuendelea kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo, ikiwemo afya, kilimo, nishati, madini, miundombinu, elimu na utalii.

Dhamira hiyo imeelezwa wakati Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Luswetula (Mb), alipokutana na kufanya mazungumzo na Naibu Katibu wa Hazina ya Marekani anayeshughulikia Masuala ya Kimataifa, Bi. Erin Browne, mjini Nairobi, Kenya, kando ya Jukwaa la Mazungumzo ya Ngazi za Juu la Mawaziri wa Fedha kuhusu kuimarisha uwekezaji wa pamoja katika sekta ya afya.

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Luswetula amezialika kampuni na wawekezaji kutoka Marekani kutumia fursa mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana Tanzania, akitaja maeneo ya kilimo, nishati, madini, miundombinu, afya, elimu na utalii.

Aidha, Mhe. Luswetula ameishukuru Serikali ya Marekani kwa kuendelea kushirikiana na Tanzania pamoja na mchango wake katika maeneo mbalimbali ya maendeleo tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mwaka 1968.

Amesema ushirikiano huo umekuwa na mchango katika juhudi za Tanzania za kukuza maendeleo ya kijamii na kiuchumi na kupunguza umaskini.

Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Hazina ya Marekani anayeshughulikia Masuala ya Kimataifa, Bi. Erin Browne, amesema Marekani itaendelea kushirikiana na Tanzania katika maeneo mbalimbali ya maendeleo, pamoja na kuimarisha na kukuza ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo.

Mazungumzo hayo yameangazia pia umuhimu wa kuendelea kujenga ushirikiano wa kiuchumi na uwekezaji kati ya Tanzania na Marekani kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizo mbili.

Address

Magufuli City, Treasury Street, Mtumba
Dodoma
40468

Opening Hours

Monday 09:00 - 16:30
Tuesday 09:00 - 16:30
Wednesday 09:00 - 16:30
Thursday 09:00 - 16:30
Friday 09:00 - 16:30

Alerts

Be the first to know and let us send you an email when Wizara ya Fedha posts news and promotions. Your email address will not be used for any other purpose, and you can unsubscribe at any time.

Contact The Organization

Send a message to Wizara ya Fedha:

Shortcuts

Share