31/05/2026
Mamlaka ya udhibiti wa huduma za Nishati na maji( EWURA) imefanya ziara ya ukaguzi katika Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bukoba(BUWASA) kwa lengo la kutathmini utendaji kazi wa Mamlaka hiyo na kuona k**a imefikia vigezo na viwango vilivyowekwa na EWURA katika utoaji wa huduma za maji safi na usafi wa Mazingira.
Kikao hicho kilifunguliwa rasmi na Mkurugenzi Mtendaji wa BUWASA Bw.John Sirati kwa kushirikiana na timu ya EWURA, ambapo Mhandisi Joseph Ngeleja alisema kuwa ukaguzi huo unalenga kupima ufanisi wa Mamlaka katika maeneo mbalimbali ikiwemo utoaji wa huduma kwa wananchi, ubora wa maji, usimamizi wa miundombinu, ukusanyaji wa mapato pamoja na utatuzi wa changamoto za wateja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa BUWASA aliishukuru timu ya EWURA kwa kufanya ziara hiyo muhimu, akieleza kuwa tathmini hiyo ni fursa ya kujifunza na kuendelea kuboresha utendaji kazi wa Mamlaka ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora, salama na endelevu.
“Mamlaka itaendelea kushirikiana kwa karibu na EWURA katika kuhakikisha viwango vya utoaji huduma vinaendelea kuimarika. Tathmini hizi zinatusaidia kuongeza uwajibikaji, uwazi na ufanisi katika kuwahudumia wananchi wetu,” alisema Bw John Sirati Mkurugenzi Mtendaji wa BUWASA.
Aidha, kikao hicho kilihusisha majadiliano mbalimbali kuhusu namna ya kuendelea kuboresha huduma za maji safi na usafi wa Mazingira kwa wananchi wa Bukoba sambamba na kuzingatia vigezo na miongozo inayotolewa na EWURA.
Timu hii iko Mkoani Kagera kwa ziara ya siku Tatu.
IMETOLEWA NA KITENGO CHA MAWASILIANO NA UHUSIANO, BUWASA
29/05/2026