21/02/2025
TAWIRI YAINGIA UWANDANI KUDHIBITI KERO YA MAMBA WILAYANI KOROGWE
Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori (TAWIRI) kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii inaendelea na kazi ya kubaini maeneo ya kujenga vizimba vya kuzuia Mashambulizi ya Mamba kwa Wananch katika kijiji cha Kwaisewa ambapo ni miongoni mwa maeneo yenye changamoto ya hofu ya wananchi kushambuliwa na Mamba.
Timu ya wataalamu ikiongozwa na Dkt. Janemary Ntalwila, Mkuu wa Kitengo cha habari na Elimu na Mtaalamu wa kudhibiti migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori akiambatana na Revocatus Meney, Mtafiti na mtaalamu wa kudhibiti migongano baina ya Binadamu na Wanyamapori inashirikiana na viongozi wa Wilaya na Kijiji cha Kwaisewa katika upimaji na uhakiki wa eneo la ujenzi wa Kizimba cha Mamba katika mto Pangani kijijini hapo.
Akizungumza na Viongozi wa Kijiji na wananchi wanaoathirika,
Dkt. Janemary ametoa wito kwa wanakijiji cha Kwaisewa kushirikiana na timu sambamba na kuzingatia maelekezo ya matumizi ya Kizimba kitakapokamilika ili kuwa na tija kwa kupunguza athari za mamba.
Naye mtafiti Revocatus Meney ametoa rai kwa wananchi kushiriki kwa dhati ili mafundi wabobezi kukamilisha ujenzi wa vizimba ndani ya muda mfupi.
Mwisho, ujenzi wa vizimba vya kuzuia mamba katika kijji cha Kwaisewa upo hatua ya pili ya upimaji wa eneo hatarishi na uwekaji alama za eneo Kizimba kitakapojengwa.