16/04/2026
Maonesho ya Kimataifa kuhusu Maendeleo ya Kilimo na Ubidhaishaji (The International Conference on Branded Agriculture Development) yalifanyika katika Mji wa Dongguan, Jimbo la Guangdong, kuanzia tarehe 11 hadi 13 Aprili 2026. Maonesho hayo yalijumuisha wadau wakuu kutoka sekta ya biashara ya kilimo, watunga sera, na wawekezaji kutoka kote duniani, na yalilenga kujadili mikakati ya kujenga chapa (brand) imara za mazao ya kilimo, kuboresha minyororo ya thamani, na kukuza bidhaa bora za kilimo zinazoweza kushindana sokoni.
Kwa upande wa Tanzania, Ofisi ya Konseli Kuu ilishiriki katika mkutano wa ufunguzi wa maonesho hayo, ambapo washiriki walipata fursa muhimu ya kujifunza teknolojia za kisasa za kilimo, mbinu za kutengeneza brand, na ufungashaji wa bidhaa, pamoja na kuimarisha uhusiano wa kibiashara na masoko ya China na kimataifa.
Fursa hii inagusa moja kwa moja wazalishaji, wachakaji, wafungashaji, na wauzaji wa mazao ya kilimo ambayo tayari yamepata soko nchini China, k**a vile kahawa, chai, korosho, mazao ya bahari, na mazao ya bustani. Kupitia kujifunza kuhusu brand zenye nguvu kimataifa, wadau hawa wataweza kubadilisha mitazamo ya biashara na kuleta tija, kuvutia mauzo ya nje, kuvutia uwekezaji, na kuchangia maendeleo endelevu ya sekta ya kilimo nchini Tanzania.